Hassan Hashim Tanga.
Chama cha wafanyakazi wa
serikali za mitaa TALGWU kimeitaka Serikali kuacha ubaguzi katika malipo ya makato
ya msingi ya watumishi wa halmashauri ambayo yamesababisha kukosa huduma za muhimu
ikiwemo matibabu huku baadhi ya kada zikilipwa kwa utaratibu stahiki.
Kauli hiyo imetolewa na
Katibu mkuu wa TALGWU Rashid Mtima wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa
habari baada ya kutembelea Halmashauri za mkoa wa Tanga na kubaini malimbikizo
ya madai ya zaidi ya shilingi bilioni nne.
Amesema utaratibu huo wa kulipa
wafanyakazi kupitia vyanzo vya ndani ukiachiwa uendelee utajenga matabaka ya kibaguzi baina ya wafanyakazi na kupunguza
tija na ari katika utendaji.
Akizungumzia utaratibu
unaotumika kwa mfanyakazi aliyeongeza ujuzi Mtima amesema muundo unaotumika wa
kurudishwa chini katika daraja la mshahara ni uonevu kwa sababu mtumishi
alishajenga uzoefu katika muda aliofanya kazi kabla ya kuongeza ujuzi.
Amesema chama cha
wafanyakazi wa serikali za mitaa kimejipanga kupigania haki za watumishi ili
kuongeza ari na kuleta maendeleo ikiwa
ni kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano.
………………………………..
|
No comments: